SALAMU ZA MWAKA MPYA KUTOKA KWA RAIS JAKAYA KIKWETE : ELIMU YA SEKONDARI BURE KUANZIA 2016

Jakaya KikweteRais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete amelihutubia Taifa, Tarehe 31 Desemba, 2014 na kuzichambua sekta mbalimbali kama vile za Elimu, Ujenzi wa maabara, Umeme, Chakula, mfumuko wa Bei, Ujangili, Dawa za kulevya, mapato ya Serikali, Dawa za kulevya na mapato ya Serikali. Isome hapo chini

Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Kama ilivyo ada imefikia siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwaka mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015. Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa ndugu na jamaa zetu ambao hawakujaliwa kuiona siku ya leo tuzidi kuwaombea mapumziko mema. Nasi tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema atujaalie umri mrefu, afya njema na mafanikio tele kwa kila tuliombalo katika mwaka 2015 na miaka ijayo.

Ndugu wananchi;
Hizi ni salamu zangu za mwisho za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi yetu. Mwakani salamu kama hizi zitatolewa na Rais wetu mpya. Mimi wakati huo nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga nikifuatilia kwenye TV na radio hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu akitoa salamu zake za kwanza za mwaka mpya, itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa kwangu.

Elimu
Jambo jipya sana na la kihistoria katika Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa ada katika elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule za msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari.

Ujenzi wa Maabara
Ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari za Kata 3,463 umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa zijengwe maabara 10,389 ilipofika Novemba, 2014. Hadi kufikia Desemba 29, 2014, maabara 4,207 sawa na asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688 sawa na asilimia 54.8 zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na maabara 494 sawa na asilimia 4. zilikuwa katika hatua za awali za ujenzi.

Umeme
Hivi sasa wananchi milioni 17.3 nchi nzima sawa asilimia 36 wamefikiwa na huduma ya umeme ikilinganishwa na watu milioni 8.1 sawa na asilimia 18.4 waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015 tunatarajia watu milioni 18.2 sawa na asilimia 38 watafikiwa na umeme.

Chakula
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini. Uzalishaji ulikuwa tani milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni 14.38 mwaka wa jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni 1.64. Kwa mujibu wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani milioni 3.25.

Mfumuko wa Bei
Mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014 ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwa asilimia 6.0. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa bei utaendelea kushuka na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.

Ujangili
Kwa ujumla kasi ya ujangili imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa ikilinganishwa na ndovu 219 waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473 mwaka 2012. Aidha, majangili 1,354 wamekamatwa na pembe za ndovu 542 na silaha mbalimbali 184 nazo zilikamatwa.

Dawa za Kulevya
Mwaka huu watuhumiwa 935 wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19 zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine, kilo 45 za cocaine na kilo 81,318 za bangi zimekamatwa.

Mapato ya Serikali
Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba, 2014 yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama hicho mwaka 2013 hadi shilingi bilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo yalikuwa asilimia 90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 4,459.7.

Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko salama na hakuna tishio lolote la kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi yetu. Uhusiano wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani ni mzuri. Hakuna nchi iliyo adui au tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha usalama wa Tanzania. Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa salama.
Uhalifu Unapungua

Ndugu Wananchi;
Taarifa za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu vimepungua ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa Polisi yalikuwa 64,088 ikilinganishwa na matukio 66,906 katika mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na raia wema. Naomba ushirikiano huu uendelee mwaka ujao na miaka ijayo ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.

Ajali za Barabarani
Ndugu Wananchi;
Nimefarijika kusikia pia kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini nayo yanaendelea kupungua. Mwaka huu kumetokea ajali 14,048 zilizosababisha vifo vya watu 3,534 na wengine 16,166 kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali 22,383 zilizosababisha vifo 3,746 na majeruhi 19,433. Hivyo mwaka huu kulikuwa na ajali 8,335, vifo 212 na majeruhi 3,267 pungufu kuliko mwaka jana. Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo ingawa bado ni nyingi mno. Naomba yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha kupata unafuu huu mwaka huu yaendelezwe maradufu mwaka 2015 na miaka ijayo.

Ugaidi
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia mabomu na kumwagia watu tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu 112 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wametiwa nguvuni. Tayari watuhumiwa 87 kati yao wameshafikishwa mahakamani na waliosalia watafikishwa wakati wo wote. Uchunguzi unaendelea ili kuwatambua wahusika wengine ambao hawajakamatwa.
Ndugu wananchi;

Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya kutambua mtandao wa ugaidi nchini na kuchukua hatua thabiti za kuudhibiti. Hali kadhalika nawashukuru raia wema waliotoa taarifa zilizowezesha haya kufanyika. Hatupaswi kubweteka wala kudhani kuwa mambo yamekwisha. Lazima tuendelee kuchukua tahadhari muda wote kwani hatujui adui anapanga kufanya hujuma gani, lini na wapi.

Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa 935 wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19 zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine, kilo 45 za cocaine na kilo 81,318 za bangi zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kukabiliana na dawa za kulevya nchini kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana. Matunda ya kazi yao tunayaona. Naomba juhudi ziongezwe maradufu mwaka ujao na miaka ijayo. Serikali itaendelea kuwaunga mkono.

Ndugu wananchi;
Kama nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu. Pamoja na kupendekeza kuongeza adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, Muswada huo pia unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye nguvu cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu ukipitishwa na kuwa Sheria tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini. 

Hotuba kamili isome hapa http://eatv.tv/…/elimu-ya-sekondari-itakuwa-bure-kuanzia-20…

Credits : eatv.tv.

 

Advertisements

One thought on “SALAMU ZA MWAKA MPYA KUTOKA KWA RAIS JAKAYA KIKWETE : ELIMU YA SEKONDARI BURE KUANZIA 2016

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s