
Peter Osaze Odemwingie akishangilia bao lake huku Emmanuel Emenike(Pichani Kulia) akimpongeza kwa bashasha
Timu ya Taifa ya Nigeria maarufu kama Super Eagles wameonyesha matumaini ya kutinga hatua ya 16 bora baada ya kuwapa kipigo cha bao 1 kwa nunge Bosnia katika mchezo wa kundi ”F” uliochezwa kwenye dimba la Arena Pantanal usiku wa kuamkia leo ikiwa ni katika kipindi cha miaka 16 tangu ilipoilaza timu hiyo kwa ushindi wa bao 1 kwa bila
Katika mchezo huo, mshambuliaji tegemezi wa Stoke City, Peter Odemwingie aliweza kuipatia Nigeria bao la pekee baada ya kupigiwa pande nzuri toka kwa mshambuliaji mwenzake Emmanuel Emenike ambapo aliweza kuitumia nafasi hiyo ipasavyo na kufanikiwa kuzifumania nyavu za Bosnia.
Matokeo hayo yanaiweka Nigeria katika nafasi ya pili kwa upande wa kundi ”F” ikiwa na pointi 4 huku ikiwa imebakisha mchezo mmoja dhidi ya Argentina ambao wapo kileleni mwa kundi hilo kwa tofauti ya pointi 2.